Japan International Cooperation Agency
Share
 • 日本語
 • English
 • Français
 • Espanol
 • Home
 • About JICA
 • News & Features
 • Countries & Regions
 • Our Work
 • Publications
 • Investor Relations

Mada na Matukio

Desemba, 2010

Elimu ya Mazingira katika Shule za Masasi

pichaTakataka hutupwa karibu na nyumbani

Ili kuboresha mazingira ya kuishi wakazi au wakazi wake, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, kupitia Idara yake ya Afya, mara kwa mara hutembelea nyumba za kulala wageni na maduka kukagua usafi wa sehemu hizo. Kwa kuongezea, Halmashauri ya Wilaya inakusudia kufanya ziara za aina hiyo katika ngazi ya jamii kuanzia sasa na kuendelea.

Kwa hivi sasa katika mji wa Masasi, takataka zimezagaa sehemu nyingi, na kwa kuwa utaratibu wa uzoaji takataka haufanyi kazi ingawaje kuna magari ya kubeba takataka yanayozoa takataka, takataka zimejaa mno mitaani.

Zaidi ya hayo, kwa kuwa kuna wafanyakazi wanaozoa takataka, watu hutupa takataka ovyo tu. Ingawa Halmashauri huwaomba wafanyabiashara katika mitaa yenye maduka kuweka mapipa ya takataka, watu hawana desturi ya kutumia mapipa hayo na inaelekea itachukua muda mrefu kabla ya watu kuzoea kutupa takataka katika mapipa ya takataka. Hali bado ni ngumu Masasi.

Katika hali kama hii, ndipo tukaamua kuanzisha programu ya masomo ya elimu ya mazingira katika shule za msingi na za sekondari kwa kushirikiana na Asasi Isiyo ya Kiserikali inayoshughulikia mazingira. Asasi hii huchangia kwa kiwango kikubwa kujenga mazingira safi Mtwara, makao makuu ya mkoa wetu.

Madhumuni ya programu hii ya elimu ya mazingira ni kujenga mazingira safi katikati ya mji wa Masasi, na kukuza uelewa wa wakazi wa Masasi kuhusu afya zao na mazingira yao wanamoishi. Kwa kufanya kazi na asasi isiyo ya Kiserikali yenye uzoefu mkubwa wa programu hii, tunatumaini kuwa maafisa afya wa wilaya wa Masasi watajifunza mbinu za kutekeleza elimu ya mazingira ya afya, na kuufanyia kazi ujuzi huo mpya katika shughuli zao katika jamii pia.

Katika masomo haya mashuleni, huwa tunaanza na swali rahisi "Mazingira ni nini?" Watoto wanakuja kuelewa kuwa "chakula, mavazi na makazi" ni "mazingira", na kwamba kuzingatia mazingira ni sawa na mtu kumudu chakula, mavazi na makazi yake. Vilevile kwa njia ya majadiliano, hujifunza uainishaji wa takataka na jinsi ya kutupa takataka, mbinu za kupunguza takataka na kuzitumia tena, na kadhalika.

Sasa miezi miwili ya programu hii ya miezi mitatu imekwisha, na tumetembelea shule za msingi tano. Kwa kuzingatia dhana ya "kujifunza kwa furaha", huwa tunaandaa michezo na nyenzo za kufundishia za kimazingira, ili wanafunzi washiriki vizuri darasani.

pichaWanafunzi wanajifunza kuhusu mazingira kwa kupitia mchezo

Kwa mfano, katika "mchezo wa kuainisha takataka", kila kikundi kidogo cha wanafunzi hupata kadi zenye majina ya takataka kama vile "chupa zilizotumika " na "kikonyo cha tufaa", na kuziainisha kwa namna mbili; "zilizooza" na "zisizooza". Kisha, kutokana na takataka "zisizooza", wanazigawa katika "zinazoweza kutumika tena" na "zisizoweza kutumika tena". Kisha, kuhusu "takataka zilizoainishwa kama zisizoweza kutumika tena ", wanafunzi hujadili "Ni kweli haziwezi kutumika tena?" "Tunawezaje kutafuta njia ya kuzitumia tena? na "Tunawezaje kuishi na takataka zisizoweza kutumika tena?". Baada ya mazoezi yote haya, kila kikundi huwakilisha maoni yao na kubadilishana mawazo na wanafunzi wengine. Ilinishangaza kugundua kwamba wanafunzi wanajua vizuri jinsi ya kuvitumia tena vitu vilivyokwishatumika, ingawa wana maarifa finyu juu ya kuainisha takataka.

Tangu programu hii ianze, baadhi ya wanafunzi wametengeneza mabango yasemayo "weka mazingira yetu safi!", na wengine wameanza shughuli ya kupanda miti. Nimefurahi kuona wanafunzi na walimu wameanza kuvutiwa na masuala ya mazingira. Ingawa umebaki mwezi mmoja tu kabla ya kumalizika kwa programu hii, ningependa kutembelea shule nyingi kadri iwezekanavyo na kutumia ziara hizo kama msingi wa kupanga shughuli za siku za baadaye.

(Bi. Yumi Koyama, JOCV, Elimu ya Mazingira, Masasi)

PAGE TOP

Copyright © Japan International Cooperation Agency