Japan International Cooperation Agency
Share
 • 日本語
 • English
 • Français
 • Espanol
 • Home
 • About JICA
 • News & Features
 • Countries & Regions
 • Our Work
 • Publications
 • Investor Relations

Mada na Matukio

29 Machi, 2011

Wafanyakazi 16 wa kujitolea kutoka Japani wawasili Tanzania

picha

Tarehe 29 Machi, 2011, wafanyakazi wa kujitolea 16 waliwasili nchini kutoka Japani ambapo kulitokea maafa makubwa hivi karibuni.

Kati ya hawa 16, watano ni wataalamu wa magari na wataenda kufundisha kwenye taasisi mbalimbali kama vile Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) vya Dodoma na Mikumi, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) vya Njombe na Mtwara, na Chuo cha Usafirishaji (NIT) kilichopo Dar es Salaam.

Vijana wengine saba wataenda kufanya kazi Zanzibar, miongoni mwao ni wataalamu wa Kompyuta, Maji, Upimaji ramani, Usanifu bustani, Mapishi, Elimu ya mazoezi ya viungo, na Tiba ya viungo.

Wengine wataenda sehemu zifuatazo; Ndanda kama mwalimu wa Sayansi na Hisabati, Mtwara kama mtaalamu wa mambo ya biashara, Tanga kama msanifu bustani, na Dar es Salaam kama mtaalamu wa madawa.

Mmoja wa wafanyakazi hawa wapya, Bw. Yuji Yachidate, amekuja nchini baada ya kuona mji wake uliopo eneo la Iwate, Kaskazini mwa Japani, umeharibiwa na Tsunami. Anasema; "Nilipata mshtuko nilipopata habari ya tetemeko lililotokea maeneo ya mji wanaokaa wazazi wangu wakati nilipokuwa kwenye mafunzo ya awali huko Japani. Baada ya kujaribu kuwasiliana na wazazi wangu bila mafanikio, niliamua kurudi nyumbani haraka. Bahati nzuri, niliwakuta wazazi wangu wako salama, lakini mji nilioishi wakati nilipokuwa mdogo ulikuwa umeharibiwa kabisa na Tsunami. Katika muda huu mgumu, wazazi wangu, ndugu na marafiki walinipa moyo ili niendelee kutekeleza uamuzi wangu wa siku nyingi wa kuja kufanya kazi Tanzania. Na sasa mimi niko hapa!" Bw. Yachidate ambaye ana uzoefu wa miaka 13 kama fundi magari, ataenda kufundisha katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mtwara.

Kwa upande mwingine, Bi. Ai Fujita na Bi. Maki Hasegawa ni wasanifu bustani. Bi. Fujita ambaye ana miaka tisa katika kazi za kutengeneza bustani ndani ya majengo anasema kwamba; "Nilisikia kwamba kule nitakapofanyia kazi, yaani Tanga, ni mji unaopendeza. Nitafurahi sana kuchangia kuuboresha zaidi kwa kutumia uzuri wake wa asili."

Bi. Hasegawa ambaye alikuwa msimamizi wa ujenzi bustani kwa miaka mitano kabla ya kuja huku anaonesha shauku ya kujua Kiswahili ili afanye kazi zake vizuri huko Zanzibar.

Sasa hivi, JICA Tanzania ina wafanyakazi wa kujitolea wa JOCV sabini na sita hapa nchini. Tangu mpango huu ulipoanza mwaka 1966, jumla ya wafanyakazi 1361 kutoka Japani wametumwa huku kufanya kazi Tanzania.

PAGE TOP

Copyright © Japan International Cooperation Agency