Japan International Cooperation Agency
Share
  • 日本語
  • English
  • Français
  • Espanol
  • Home
  • About JICA
  • News & Features
  • Countries & Regions
  • Our Work
  • Publications
  • Investor Relations

Taarifa kwa Umma

10 Desemba 2021

Teknolojia mpya ya Kijapani na mtindo wa biashara umebadilisha tasnia ya viazi vitamu nchini Tanzania

"Kilimo hakina msongo wa mawazo pale mbegu, pembejeo na masoko vinakuwa vya uhakika", wakulima wa viazi vitamu Morogoro na Dodoma wamekiri.

Teknolojia na mtindo wa biashara kutoka Japani zimeondoa dhiki, ambayo ilikuwa inawakabili wakulima wa viazi vitamu.

"Kuhangaika kupata mbegu za kisasa na soko hakuna tena. Ni hali ya hewa pekee inayonisumbua na nina uhakika wa mavuno mazuri na kuuza viazi vitamu kwa bei nzuri," asema Bw Peter Chisina, mkulima wa viazi vitamu kutoka Gairo, Morogoro, mkulima wa mkataba na kampuni ya Matoborwa Co. Ltd.

Teknolojia hiyo na mtindo wa biashara ulianzishwa nchini Tanzania na Bw. Tatsuo Hasegawa, aliyekuwa mjapani wa JICA kutoka Mpango wa wajapani wa kujitolea (JOCV) ambaye alianzisha kampuni ya Matoborwa. mjini Dodoma mwaka 2014.

Ikiwa na mtaji wa awali wa dola za Marekani 96,000 (TSh165 milioni), dira ya kampuni hii ni kutengeneza chakula bora na chenye virutubisho kwa bei nafuu kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.

Kiwanda kinazalisha vitafunio vya viazi vitamu vilivyokaushwa, matunda yaliyokaushwa na kashata za kokwa. Hivi sasa kampuni imeajiri takribani Watanzania 15 ambao wengi wao ni akina mama wasio na waume. Wafanyakazi hawa wanafanya kazi kwa kujituma kama Wajapani. Kwa kufanya kazi kampuni ya Matoborwa wameweza kumudu mahitaji yao ya kimsingi ikiwa ni pamoja na chakula na elimu kwa watoto wao.

"Maendeleo ya kilimo barani Afrika yamegeuka kuwa kazi yangu ya maisha," anasema Bw. Hasegawa, "na uzoefu wangu kama JOCV ulinifanya kuchagua Tanzania kama kivutio changu cha uwekezaji. Nikiwa na umri wa miaka 24 nilipokuja Tanzania kama Mjapani wa kujitolea, nilijifunza lugha ya Kiswahili na kupata marafiki wengi wa Kitanzania".

Bw. Hasegawa, ambaye alisoma katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa udhamini wa JICA, amechagua viazi vitamu vya Kijapani vinavyoitwa "Tamayutaka" kwa ajili ya Watanzania. Anasema aina hiyo inafaa kwa mazingira ya Tanzania na haihitaji mbolea wala dawa. Aina hii ilisajiliwa nchini Tanzania mwaka 2020 kwa usaidizi wa kifedha na kiufundi kutoka JICA.

Mkulima wa mkataba kutoka Mpwapwa, Dodoma Bw.Saimon Mlali alisema kwamba maisha yake yalibadilika mara baada ya kuanza kufanya kazi na kampuni ya Matoborwa mwaka 2018. Kwa kutumia mtindo wa kibiashara kutoka Japani, kampuni ya Matoborwa inatoa mbegu na ujuzi wa kulima kwa wakulima na kununua bidhaa zao kama malighafi za kulisha kiwanda - mfumo ambao unathaminiwa zaidi na wakulima kwa sababu wana uhakika wa soko lililo tayari kwa ajili ya mazao yao.

Mwanzilishi mwenza wa kampuni hiyo, Bw.Crispin Sukwa, mkurugenzi na rafiki wa muda mrefu wa Bw. Hasegawa tangu mwaka 1995, anasema uwezo wa kiwanda hicho umelingana na uzalishaji na usambazaji uliopo wa malighafi kulingana na mahitaji ya soko.

"Tunanunua malighafi, kulingana na uwezo wetu wa uzalishaji. Mipango ipo ya kufunga mashine mpya ili kukidhi mahitaji," anabainisha.

Kuhusu Wafanyakazi wa Kujitolea kutoka Japani (JOCV)

JOCV ni mpango chini ya Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA). JOCV ilianza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1967 na kufikia Machi 2020 zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea wa Japani 1,700 akiwemo Bw. Hasegawa walikuwa wametumwa kufanya kazi katika sekta na maeneo mbalimbali ya Tanzania. Mpango huo unalenga kusaidia nchi zinazoendelea kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kusisitiza kujitegemea kwa mabadiliko endelevu katika sekta mbalimbali.

Kuhusu Mr. Tatsuo Hasegawa

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Matoborwa Co.Ltd. Alipata M.A. katika Chuo Kikuu cha Kyoto, Japani. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa miaka miwili (1999-2001). Ana uzoefu wa kufanya kazi katika tasnia ya chakula, kampuni ya uchapishaji wa kilimo, ushauri, n.k. nchini Japani. Alianzisha Kampuni ya Matoborwa. mjini Dodoma. Kwa ushirikiano na wakulima wa ndani, Bw. Hasegawa anajaribu kuunda sekta ya usindikaji wa chakula, ambayo itazalisha bidhaa za hali ya juu za ushindani kwa ajili ya soko

Kuhusu kampuni ya Matoborwa Co.Ltd.

Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka wa 2014 nchini Tanzania, ilisajili viazi vitamu vya Kijapani vinavyoitwa ‘Tamayutaka’ na kuzalisha viazi vitamu vilivyokaushwa. Sasa bidhaa zao ziko katika maduka makubwa makubwa nchini Tanzania. Kampuni imedhamiria kufanya kazi pamoja na wakulima ili kuboresha ubora wa viazi vitamu vilivyokaushwa vyema. Kampuni inajitahidi kuendelea kutoa huduma bora na zenye gharama nafuu kwa wateja wake waliopo nchini Tanzania na Japani.

PhotoBwana Hasegawa anakagua maendeleo ya shamba la viazi vitamu, Dodoma, pamoja na wakulima mwaka 2017


Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na:
JICA Tanzania Office, P.O. Box 9450,
Dar es Salaam, Tel: 022-211327/30
Ms. Noriko Ogasa: jicatz-vcs@jica.go.jp
Ms. Catherine Shirima: ShirimaCatherine.Tz@jica.go.jp

PAGE TOP

Copyright © Japan International Cooperation Agency