Ujumbe kutoka kwa Mwakilishi Mkuu

Niliwasili nchini Tanzania kama Mwakilishi Mkuu wa Ofisi ya JICA Tanzania mwezi Februari 2023.

Ujio wangu katika nchi hii nzuri ulikuja miezi miwili tu baada Ofisi ya JICA Tanzania kusherehekea miaka 60 ya shughuli zake hapa nchini.

Ingawa nchi hii ina makabila zaidi ya 120, nchi hii ina umoja na inaelekea hakuna ukabila miongoni mwa wananchi wake. Aidha Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali watu na maliasili. Isitoshe amani na utulivu vimetamalaki nchini. Hali ya utulivu niliyoikuta hapa nchini kwa kweli inatamanisha.

Uhusiano wa JICA na Tanzania ulianza mwaka 1962, yaani mwaka mmoja tu baada ya uhuru wa Tanganyika, pale mtumishi mmoja wa Serikali ya Tanzania alipopokelewa kwa mafunzo nchini Japan. Tokea wakati huo ushirikiano huo uliendelea kukua na kujumuisha si tu ushirikiano wa kiufundi na uletaji wa wataalam wa kujitolea (JOCV), bali pia utoaji wa mikopo na pia misaada isiyolipiwa.

Photo

Katika miaka 60, idadi ya Watanzania waliosomeshwa chini ya ufadhili wa JICA imezidi 22,000 na pia tumefanyakazi na Watanzania wengi sana. Hazina zetu katika ushirikiano huu ni uzoefu wetu katika nyanja mbalimbali za kiufundi na kifedha na pia kupitia mpango wa wataalam wa kujitolea kutoka Japan (JOCV).

Aidha Mkutano wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD), ambao unasisitiza umuhimu wa maendeleo ya Afrika kusimamiwa na Waafrika wenyewe na pia ushirikiano wa kimataifa, pia ulitimiza miaka 30 mwaka jana, na JICA nayo inajishughulisha kwa kasi kusaidia katika maendeleo ya Afrika na Tanzania.

Kutokana na historia hiyo ni heshima na pia ni changamoto kwangu kushika nafasi hii kwa sasa.

Kwa muongo mmoja sasa Tanzania imeshuhudia ukuaji mzuri wa uchumi na pia utulivu wa kiuchumi pamoja na mabadiliko ya sera. Aidha Tanzania iliweza kua na uchumi wa kati Julai 2020, miaka mitano kabla ya mwaka 2025, mwaka ambao ilitarajiwa ingefikia hatua hiyo.

Kwa upande mwingine, Tanzania ina changamoto nyingi kufikia maendeleo endelevu kama vile hali isiyoridhisha katika viwanda, miundombinu, umaskini, usimamizi wa rasilmali fedha za umma, tabia nchi n.k.

Katika dunia iliyo na changamoto nyingi zisizotabirika ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, umuhimu wa jamii ya kimataifa kuungana kupigana na changamoto hizo ni jambo la msingi kabisa.

Ofisi ya JICA Tanzania ina dhamira ya kuongeza kasi na ubora wa ushirikiano na Tanzania si tu na Serikali ya Tanzania bali pia na sekta binafsi za Japan na Tanzania, washirika wa maendeleo na pia na Watanzania wote.

ARA Hitoshi
Mwakilishi Mkuu
Ofisi ya JICA Tanzania
Machi 6, 2023