Japan International Cooperation Agency
Share
  • 日本語
  • English
  • Français
  • Espanol
  • Home
  • About JICA
  • News & Features
  • Countries & Regions
  • Our Work
  • Publications
  • Investor Relations

Taarifa kwa Umma

17 Machi 2022

JICA na Wilaya ya Mkuranga zakuza Mpango wa Afya Shuleni

Angalau shule 22 kati ya 30 za sekondari za umma katika Wilaya ya Mkuranga zinafanya ‘programu za afya shuleni' ambapo shule zinapatiwa vyumba vya huduma maalum za afya na walimu wa afya waliohitimu ambao wana wajibu wa kuangalia hali za afya za wanafunzi

Kwa mujibu wa Afisa Elimu wa Wilaya wa Shule za Sekondari Bw. Benjamin A. Majoya, wazo la asili la kuanzishwa kwa mfumo huo wa huduma za afya lilitoka Japani na lililetwa kwa mara ya kwanza wilayani humo na Bi. Azusa OSAWA ambaye alikuwa mtaalam wa kujitolea kupitia Mpango wa Wataalam wa Kujitolea kutoka Japani n (JOCV) ambaye alihudumu hapa nchini kutoka 2011 hadi 2013.

Baada ya mafunzo yake nchini Japani chini ya ufadhili wa Mpango wa Mafunzo wa JICA (KCCP), mwaka wa 2014, Bw. Majoya alifanya kazi kwa karibu na Wajapani wengine wawili wa kujitolea wa JICA (Bi. Keiko Ito na Bi. Yuna Honda) wa programu hiyo ya JOCV.

Mpango huu wa afya hutoa manufaa makubwa kwa wanafunzi na walimu. "Mpango huu unasaidia wanafunzi hasa wa kike kufahamu hali zao za kiafya wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali wakati wa ujana wao" alisema na kuongeza: "Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga inatoa huduma ya kwanza ikiwa ni pamoja na ushauri na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ili waweze kufahamu mabadiliko ya kibaiolojia katika maisha yao na miili yao".

Katika hatua nyingine Bw. Majoya ametaka mpango huo uenezwe nchi nzima kwa kuwa umechangia kwa kiasi kikubwa ufaulu wa wanafunzi katika wilaya yake.

Pia aliishukuru JICA kwa kuwaletea Wajapani wengine wawili, Bi. Keiko Ito kutoka 2013-2016 na Bi. Yuna Honda kutoka 2019 hadi 2020 na kuongeza kuwa, Wajapani hao watatu wa kujitolea walifanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia uhifadhi wa wakati na utendaji wao kwa ujumla ulistahili kuigwa na wilaya yake yote.

Kwa upande wake mnufaika mwingine wa mafunzo ya JICA, Mwalimu Halima Omary, mwalimu wa sayansi katika Shule ya Sekondari Kiparang'anda, alipongeza mpango huo akisema unalenga kuwawezesha wanafunzi kujua namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika ukuaji wao na hivyo kuweza kusimama kidete kufikia malengo yao ya kikazi ili kukamilisha masomo yao vizuri.

Katika hatua nyingine, Bi. Yuna Honda na Mjapani mwingine wa kujitolea, Bi. Naoko Shiosaki (aliyefanya kazi Dodoma), wametengeneza video kwa lugha ya Kiswahili kuhusu afya ya ujana hasa kwa wasichana inayoitwa, Balehe-Kuvunja ungo kwa wasichana:

Kutokana na janga la Uviko - 19, wawili hao walilazimika kuondoka Tanzania mwaka 2020. Wakiwa nchini Japani walitengeneza video hii kutokana na kile ambacho Bi Honda alikuwa akifundisha huko Mkuranga.

Maafisa watatu wa Mkuranga walipata mafunzo nchini Japani kupitia mpango wa ushirikiano wa mafunzo ya JICA na kujiunga na kozi ya afya shuleni. Walichunguza na kujifunza mfumo wa elimu wa Japani na kuuingiza katika wilaya hiyo.

PhotoBw.Benjamin Majoya, Afisa Elimu Wilaya, Mkuranga

PhotoHuduma ya Kwanza, Kiparang'anda Sekondari


Kuhusu Mpango wa Wataalam wa Kujitolea kutoka Japani (JOCV) :

JOCV ni programu chini ya Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA). JOCV ilianza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1967 na kufikia Machi 2020, zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea wa Japani 1,700 walikuwa wametumwa kufanya kazi katika sekta na maeneo mbalimbali ya Tanzania. Mpango huo unalenga kusaidia nchi zinazoendelea kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kusisitiza kujitegemea kwa mabadiliko endelevu katika sekta mbalimbali

Kuhusu Mpango wa Ushirikiano katika kukuza Maarifa (KCCP) :

Mpango wa Ushirikiano katika kukuza Maarifa wa JICA yaani KCCP ni aina ya ushirikiano wa kiufundi ambao JICA inatekeleza nchini Japani, katika nchi ya tatu au mtandaoni. Baadhi ya maarifa ambayo jamii ya Kijapani imekusanya, ikiwa ni pamoja na uzoefu wake katika maeneo kama vile ujuzi wa shirika na mifumo ya kijamii, yanaweza kueleweka kwa ufanisi zaidi kupitia uzoefu wa kibinafsi. Mipango ni njia muhimu ya ushirikiano wa kiufundi ambayo inasaidia maendeleo ya rasilimali watu na kutatua masuala katika nchi zinazoendelea.

Kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya Afrika (TICAD 8) :

TICAD ni mkutano wa kimataifa unaohusu maendeleo ya Afrika. Mkutano wa kwanza (TICAD1) ulifanyika mwaka wa 1993 chini ya uongozi wa serikali ya Japani. Mwezi Agosti 2022, TICAD ya 8 itafanyika Tunisia. Hii itakuwa ni mara ya pili kwa TICAD kufanyika barani Afrika, kufuatia TICAD 7 iliyoandaliwa na Kenya mwaka 2016. JICA inalenga kusaidia maendeleo ya Afrika kuelekea bara lenye uthabiti, shirikishi na lenye ustawi.

About TICAD :

Kwa maelezo Zaidi wasiliana na :
JICA Tanzania Office, P.O. Box 9450,
Dar es Salaam, Tel: 022-211327/30
Ms. Noriko Ogasa: jicatz-vcs@jica.go.jp
Ms. Catherine Shirima: ShirimaCatherine.Tz@jica.go.jp

PAGE TOP

Copyright © Japan International Cooperation Agency