Japan International Cooperation Agency
Share
  • 日本語
  • English
  • Français
  • Espanol
  • Home
  • About JICA
  • News & Features
  • Countries & Regions
  • Our Work
  • Publications
  • Investor Relations

Taarifa kwa Umma

14 Desemba 2020

Mshauri Mkuu wa zamani wa Mradi wa Ushirikiano wa Kitaalam wa Kilimo cha Mpunga wa JICA apokea Tuzo ya Pongezi ya Waziri wa Mambo ya nje wa Japani.

"Nilijifunza teknolojia za kilimo cha mpunga kutoka kwa Mjapani ambaye alikuwa anaitwa Bwana Tomitaka. Tangu wakati huo nimekuwa nikitumia teknolojia kama hizo kuzalisha mchele zaidi na bora kuliko hapo awali ", mkulima wa mpunga katika Wilaya ya Kilombero alisema.

Bwana TOMITAKA Motonori, ni Mshauri Mkuu wa zamani wa Mradi wa Ushirikiano wa kitaalam kati ya Tanzania na Japani uitwao "Mradi wa Kuendeleza zao la Mpunga katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (TANRICE2)" ambao uilitekelezwa kwa pamoja kati ya Wizara ya Kilimo (MoA) na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA). Bwana Tomitaka ni mmoja wa wapokeaji wa Tuzo ya Pongezi ya Waziri wa Mambo ya nje wa Japani mnamo 2020.

Bwana Tomitaka amefanya kazi kuleta maendeleo ya kilimo, hasa katika kukuza na kuendeleza kilimo cha mpunga katika nchi za Afrika, kama Mtaalam wa JICA tangu mwaka 1983. Kwa karibu miaka 20 tangu mwaka 1986 alikuwa akifanya kazi katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro (KATC) ambacho ni kituo kilicho chini ya Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji. Mchango wake mkubwa ulikuwa katika kusimamia mfululizo wa miradi ya ushirikiano wa kiutaalam kati ya Wizara ya Kilimo na JICA. Kipekee alisisitiza hasa juu ya utoaji wa huduma za kuwafikia wakulima moja kwa moja mashambani kwao, ili wakulima kama hao waweze kujifunza teknolojia zinazofaa kwa mazingira yao wenyewe. "Teknolojia hizo za kilimo cha mpunga", ikiwa ni pamoja na upandikizaji wa moja kwa moja, kutengeneza matuta ili kupata maji, kusawazisha mashamba ili kuhifadhi maji sawasawa katika mashamba, uchaguzi wa mbegu, n.k. ambazo zilistawishwa KATC huko Kilimanjaro, baadaye zilisambazwa nchini kote. Mbali na utoaji wa teknolojia kama hizi za kilimo cha mpunga, TANRICE2 pia ilitoa mipango kadhaa maalum ya mafunzo juu ya "usimamizi wa skimu za umwagiliaji", "jinsia", "masoko/uuzaji", "zana za kilimo", n.k., zote zikiwa zinalenga katika kuongeza uzalishaji wa mpunga na kwa hivyo kuboresha maisha ya watu wanaoishi vijijini. Sasa, kwa sababu ya juhudi hizi za Wizara ya Kilimo na wakulima wote wa vijijini uzalishaji wa mpunga nchini Tanzania uliongezeka mara 6 katika miaka 20, yaani kutoka tani milioni 0.5 mwaka 1986 hadi tani milioni 3.0 mwaka 2018 (FAOSTAT), ambayo ni ongezeko la ajabu sana.

Ingawa Bwana Tomitaka amewahi kufanya kazi nchini Tanzania, pia alifanya kazi nchini Thailand, Ghana, na Uganda kama mtaalam wa kukuza na kuendeleza kilimo vijijini katika nchi hizo.

Tuzo za Pongezi za Waziri wa Mambo ya nje wa Japani zinapewa watu binafsi na vikundi vya watu wenye mafanikio bora katika nyanja za kimataifa, ili kutambua michango yao katika kukuza urafiki kati ya Japani na nchi washirika / maeneo mbalimbali. Tuzo hizo pia zinalenga kukuza maelewano baina ya Japani na nchi/eneo husika. Mwaka jana, Dk Edwin Mhede, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alikuwa mmoja wa waliopokea Tuzo hizi za Pongezi.

Mnamo mwaka wa 2020, Pongezi zilitolewa kwa vikundi 65 na watu 172, pamoja na Bwana Tomitaka, ambaye alichaguliwa kama mmoja wa wapokeaji hao kwa kutambua sana mchango wake katika kukuza ushirikiano wa kiufundi wa kimataifa. Bwana Tomitaka alisema, "Ninapokea Pongezi hii kuwathamini wakulima wote wa Tanzania."

PhotoBwana Tomitaka, akielezea aina ya mpunga kwa washiriki kutoka Misri huko KATC- Kilimanjaro, Desemba 2017. Kwa sababu Tanzania ni moja ya nchi kuu kwa uzalishaji wa mpunga, idadi kubwa ya washiriki wa mafunzo kutoka nchi zingine za Kiafrika wamekuwa wakitembelea KATC kujifunza mafanikio yake katika kuongeza uzalishaji wa mpunga nchini.


  • Kuhusu JICA (Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani)

Hili ni Shirika la Serikali ya Japani linalosimamia Misaada Rasmi ya Maendeleo inayotolewa na Serikali ya Japani. Ni moja ya mashirika makubwa zaidi duniani yanayotoa misaada ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya nchi zinazoendelea na maeneo mbalimbali duniani.

Nchini Tanzania, JICA imekuwa mshirika wa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 50 katika sekta nyingi tangu 1962.


Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:
JICA Tanzania Office, P.O. Box 9450, Dar es Salaam,
Tel: 022-2113727/30 Fax: 022-2112976
Ms. YAMADA Namiko / 0682215969 / Yamada.Namiko@jica.go.jp
Ms. Ridda A. Dally / 0699806920 / Andrew-Ridda@jica.go.jp

PAGE TOP

Copyright © Japan International Cooperation Agency